Exodus 28:31-43

Mavazi Mengine Ya Kikuhani

(Kutoka 39:22-31)

31 a“Shona joho la kisibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu, 32na katikati uweke nafasi ya kuingizia kichwa. Kutakuwa na utepe uliofumwa, unaofanana na ukosi kuizunguka nafasi hiyo, ili isichanike. 33 bTengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu kuzunguka pindo la hilo joho, na uweke pia vikengele vya dhahabu kati ya hayo makomamanga. 34Hivyo vikengele vya dhahabu na makomamanga vitapishana kuzunguka upindo wa joho lile. 35Ni lazima Aroni alivae anapofanya huduma. Sauti ya hivyo vikengele itasikika anapoingia na kutoka Mahali Patakatifu mbele za Bwana, ili asije akafa.

36 c“Tengeneza bamba la dhahabu safi na uchore juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa: Mtakatifu kwa Bwana. 37Lifunge hilo bamba kwa kamba ya buluu kwenye kilemba, nalo ni lazima liwe mbele ya kilemba. 38 dAroni alivae bamba hilo kwenye paji la uso wake, naye atachukua hatia kuhusu sadaka takatifu za Waisraeli wanazoweka wakfu, sadaka za aina yoyote. Litakuwa kwenye paji la uso wa Aroni daima ili zikubalike kwa Bwana.

39 e“Fuma koti la kitani safi na ufanye kilemba cha kitani safi. Mshipi uwe ni kazi ya mtarizi. 40 fWatengenezee wana wa Aroni makoti, mishipi na kofia, ili kuwapa ukuu na heshima. 41 gBaada ya kumvika Aroni ndugu yako pamoja na wanawe nguo hizi, watie mafuta na kuwabariki. Waweke wakfu ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.

42 h“Watengenezee nguo za ndani za kitani zitakazofunika mwili, kutoka kiunoni hadi mapajani. 43 iAroni na wanawe ni lazima wavae haya kila wanapoingia katika Hema la Kukutania au wanaposogelea madhabahu wakati wa kutoa huduma katika Mahali Patakatifu, ili wasije wakafanya kosa wakafa.

“Haya yawe maagizo ya kudumu kwa Aroni na vizazi vyake.

Copyright information for SwhNEN